Refugee Advisory Council Application (Swahili)

A refugee resettlement caseworker helping two recently resettled refugees at his office in Baltimore

Kushiriki katika Baraza la Kutoa Ushauri kwa Wakimbizi la Shirika la CORE


CORE ni mpango wa usaidizi wa kiufundi ambao huunganisha na kusaidia wafanyakazi wa kutoa huduma za kuwapa wakimbizi makazi mapya duniani kote ili kutoa huduma bora ya maelezo kuhusu Mwelekeo wa Utamaduni. Tunashirikiana na Vituo vya Usaidizi wa Kupata Makazi Mapya (RSC) na Mashirika ya Huduma za Kupata Makazi Mapya (RA) ili kuboresha huduma ya kutoa maelezo kuhusu Mwelekeo wa Utamaduni ambayo wakimbizi hupokea kabla ya kusafiri na baada ya kuwasili Marekani. Kwa sasa tunaandikisha watu wa kujiunga na Baraza la Kutoa Ushauri kwa Wakimbizi la Shirika la CORE na tunatafuta watu ambao wangependa kushiriki.   

Mpango na Muhtasari wa Kazi:

Mpango wa Cultural Orientation Resource Exchange (CORE) unaotekelezwa na IRC, ni mpango wa usaidizi wa kiufundi ambao huunganisha na kusaidia wafanyakazi wa kutoa huduma za kuwapa wakimbizi makazi mapya duniani kote ili kutoa huduma bora ya maelezo kuhusu Mwelekeo wa Utamaduni (CO) ambayo husaidia wakimbizi kuzoea maisha nchini Marekani. Kama sehemu ya kazi hii, shirika la CORE husimamia na kudhibiti tovuti ya CORE, ambayo ni mfumo wa mafunzo, tovuti ya Resettlement Navigator, na programu ya simu ya Settle In. Shirika la CORE linafadhiliwa na Idara ya Serikali ya Marekani, Taasisi ya Idadi ya Watu, Wakimbizi na Uhamiaji (U.S. Department of State, Bureau of Population, Refugees, and Migration).

Shirika la CORE linatafuta wakimbizi waliopata makazi rasmi ili wajiunge na Baraza la Kutoa Ushauri kwa Wakimbizi (RAC) kwa mkataba wa muda mfupi wa kazi isiyo ya wakati wote wa kipindi cha mwaka mmoja. RAC inajumuisha hadi wakimbizi 20 wa zamani waliopata makazi mapya kupitia Mpango wa Uandikishaji wa Wakimbizi Nchini Marekani (United States Refugee Admissions Program – USRAP). Kama mwanachama wa RAC, washauri waliochaguliwa watafanya kazi kwa kushirikiana na Afisa wa Mawasiliano ya Wakimbizi na wafanyakazi wengine wa shirika la CORE ili kutoa maoni mahususi na kuwafahamisha wakimbizi kuhusu mipango ya CORE kama watoa huduma za kiufundi za kutoa maelezo kuhusu Mwelekeo wa Utamaduni (CO).

Kushiriki katika RAC kunahitaji mshiriki awe na uwezo mkubwa wa ushirikiano na uwezo wa kujitolea kufanya kazi kwa wastani wa masaa 5 hadi 8 kwa mwezi kwa kipindi cha miezi 12. Hii ni kazi nzuri inayolipwa. Ni lazima washiriki wawe wanaishi Marekani na wamepata makazi mapya kupitia Mpango wa Uandikishaji wa Wakimbizi nchini Marekani (USRAP). Ili kushiriki katika RAC, lazima washiriki wawe na uwezo wa kuzungumza na kusoma kwa lugha moja au zaidi zifuatazo: Kiarabu, Kiburma, Kidari, Kiingereza, Kinyarwanda, Kirusi, Kihispania, na/au Kiswahili.

Majukumu Makuu:

 • Kushirikiana na Afisa wa Mawasiliano ya Wakimbizi, wafanyakazi wa shirika la CORE na washiriki wengine wa RAC ili kusaidia kusikika kwa maoni ya wakimbizi na kutoa maoni mahususi kuhusu mada zinazohusiana na Mwelekeo wa Utamaduni  (yaani, kupata nyumba, kuingiliana na utamaduni, kupata kazi, huduma za afya n.k.) kupitia kufanya mazungumzo na kikundi lengwa, kufanya mahojiano ya kibinafsi au kufanya majaribio mengine yanayolenga mtumiaji na/au njia za utafiti;
 • Kukagua nyenzo mapema kabla ya kuhudhuria mikutano na kutoa maoni ikiwa ni pamoja na karatasi za maelezo, video na maelezo mengine yaliyotungwa ili kutumiwa na wakimbizi wapya wanaowasili, kama inavyohitajika;
 • Kuhudhuria mikutano ya kibinafsi au ya kikundi ya kila mwezi ya mtandaoni;
 • Kukamilisha kazi za kufanyia nyumbani au shughuli za matayarisho, kushiriki katika mikutano ya simu, tafiti na kazi zingine kama ilivyofafanuliwa kwenye upeo wa mradi, kama inavyohitajika. Baadhi ya mifano ya upeo wa kazi ni pamoja na, wala si tu:
  • Kufanya majaribo ya mtumiaji kwa violesura vya mifumo ya kutumiwa na wakimbizi vya shirika la CORE, programu ya COREnav na Settle In;
  • Kufanya mazungumzo na kikundi lengwa na mahojiano ya kibinafsi kuhusiana na mada zinazohusu utofauti, usawa na ujumuishaji;
  • Kutoa maoni kuhusu nyenzo za violesura vya kutumiwa na wakimbizi vya shirika la CORE, kama vile karatasi ya maelezo na video ya shirika la CORE kuhusu “Jinsi ya Kuwasiliana na Polisi”.

Masharti ya Kazi:

 • Uwezo unaotambulika wa kufanya kazi kwa ushirikiano na kama timu;
 • Ujuzi thabiti wa mawasiliano na kuweza kutoa maoni ya wazi na ya kuaminika kama kikundi au mtu binafsi;
 • Kupenda zaidi ubunifu na uongozi wa wakimbizi katika mpango wa kuwapa wakimbizi makazi mapya, na uwezo na kupendelea kufanya kazi na shirika la CORE kama mshauri kwa kipindi kifupi;
 • Uwezo wa kujitolea kufanya kazi kwa wastani wa masaa 5 hadi 8 kwa mwezi mtandaoni kwa kipindi cha miezi 12;
 • Uwezo wa kusoma na kuandika kwa lugha moja au zaidi zifuatazo: Kiarabu, Kibama, Kidari, Kiingereza, Kinyarwanda, Kirusi, Kihispania na/au Kiswahili. Shirika la CORE litatoa huduma za ukalimani kama itakavyohitajika;

Kiwango cha msingi cha ufahamu wa masuala ya teknolojia na uwezo wa kutumia vifaa vya kidijitali ikiwa ni pamoja na uwezo wa kujiunga katika mkutano wa simu au Zoom kwa kutumia simu, kompyuta kibao au kompyuta ya kawaida yenye muunganisho thabiti wa intaneti; uwezo wa kukagua hati za mtandaoni na tovuti; uwezo wa kufanya mtandaoni.

Mazingira ya Kazi: Kazi ya kufanywa kwa mbali; huenda ukahitajika kufanya kazi jioni wakati mwingine kwa sababu ya tofauti ya saa za eneo.

Tunazingatia zaidi usawa katika kutoa fursa za kazi na tunathamini utofauti wa watu katika kampuni yetu. Hatuwabagui watu kwa misingi ya asili, dini, rangi, utambulisho wa kijinsia, mwelekeo wa kijinsia, umri, hali ya ndoa, hali ya mwanajeshi aliyestaafu au hali ya ulemavu. Tutahakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata malazi yanayofaa ili kushiriki katika shughuli ya kutuma maombi ya kazi au mchakato wa mahojiano, kutekeleza shughuli muhimu za kazi na kupokea manufaa na marupurupu mengine ya kazi. Tafadhali wasiliana nasi ili uombe malazi.

Jinsi ya kutuma maombi

Hatua ya kutuma maombi ya kushiriki katika Baraza la Kutoa Ushauri kwa Wakimbizi inahitaji ujaze na utume utafiti mfupi na uambatishe hati ya maelezo yako binafsi (CV). Ikiwa ungependa kutuma maombi ya kushiriki katika Baraza la Kutoa Ushauri kwa Wakimbizi, tafadhali kamilisha hatua zilizobainishwa hapa chini:

 1. Fungua kiungo hiki ili ufikie sehemu ya kujaza maombi ya kazi kisha uchague lugha yako. Ikiwa lugha yako haipo, unaweza kujaza maombi ya kazi kwa lugha zifuatazo: Kiarabu, Kiburma, Kidari, Kiingereza, Kinyarwanda, Kirusi, Kihispania, na/au Kiswahili.
 2. Jibu maswali ya maombi ya kazi kisha uambatishe hati ya maelezo yako binafsi (CV) kwenye maombi hayo. Ikiwa huwezi kuambatisha hati ya maelezo yako binafsi (CV) kwenye maombi ya kazi, unaweza pia kututumia moja kwa moja kupitia barua pepe katika coresourceexchange@rescue.org.
 3. Tuma maombi yako.

Baada ya kutuma maombi, tutawasiliane na watakaochaguliwa kwa ajili ya kuwahoji. Shirika la CORE litatoa huduma za ukalimani kwa ajili ya mahojiano kama itakavyohitajika. Washiriki watarajiwa wanapaswa kutaja mapema ikiwa wanahitaji huduma za ukalimani. Pia, mawasiliano yote kupitia barua pepe yatakuwa kwa lugha ya Kiingereza na shirika la CORE litatoa mawasiliano yaliyotafsiriwa kama itakavyohitajika.

Kuhusu Baraza la Kutoa Ushauri kwa Wakimbizi na Maswali Yanayoulizwa Sana

Baraza la Kutoa Ushauri kwa Wakimbizi (RAC) ni mahali rasmi pa kupata maoni kutoka kwa wakimbizi waliopata makazi rasmi kuhusu hali ya huduma ya kutoa maelezo kuhusu Mwelekeo wa Utamaduni waliyopata na jinsi wanavyoendelea baada ya kupata makazi mapya nchini Marekani. Wanachama wa RAC watasaidia kuchangia katika kuboresha huduma ya kutoa maelezo kuhusu Mwelekeo wa Utamaduni kwa wateja wa baadaye watakaopata makazi mapya kupitia mpango wa USRAP.

RAC inajumuisha kikundi cha wakimbizi mbalimbali na/au waliotuma maombi ya SIV ambao wameishi Marekani kwa miezi 6 hadi 24 iliyopita. Hapa ni mahali rasmi pa kutoa maoni mahususi kuhusu mipango na nyenzo za CORE; mahitaji ya huduma mahususi ya kibinafsi bado yanapaswa kuwasilishwa kwa Shirika la Huduma za Kupata Makazi Mapya la eneo.

Ndiyo, hii ni kazi nzuri ya kulipwa isiyo ya wakati wote. Washiriki huandikwa kutoa huduma kwa kipindi kisichozidi miezi 12. Washiriki hulipwa $40 kwa kila saa.

Ili kushiriki katika RAC, ni sharti washiriki wawe wanaishi Marekani na wamepata makazi mapya kupitia Mpango wa Uandikishaji wa Wakimbizi Nchini Marekani (United States Refugee Admissions Program – USRAP) kwa miezi 6 hadi 24 iliyopita. Si lazima washiriki wawe na ufahamu kuhusu shirika la CORE au kazi yake, lakini wanapaswa kuwa na ufahamu kuhusu mchakato wa kuwapa wakimbizi makazi mapya na, Mwelekeo wa Utamaduni, kama inavyofaa. Pia, lazima washiriki wajitolee kutoa huduma kwa kipindi cha miezi 12. Ili uone orodha kamili ya masharti, tafadhali angalia maelezo ya kazi.

Shirika la CORE linatafuta washiriki 10 hadi 12 waliopata makazi mapya kupitia Shirika la nchini la Huduma za Kupata Makazi Mapya kupitia Mpango wa Uandikishaji wa Wakimbizi Nchini Marekani (United States Refugee Admissions Program) katika kipindi cha miezi 6 hadi 24 iliyopita. Kwa njia mahususi, RAC inapaswa kuwakilisha mitazamo mbalimbali. Kwa sababu hiyo, shirika la CORE linatafuta washiriki wa umri wa kati ya miaka 18 na 64, kutoka katika kila maeneo yafuatayo:

 • Mashariki ya Kati
 • Mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara
 • Ulaya Mashariki
 • Kusini Mashariki mwa Asia na Afghanistani
 • Marekani Kusini

Washiriki wenye hali mbalimbali na halisi wanahimizwa kutuma maombi. Hali mbalimbali na halisi zinaweza kuwa ni pamoja na, wala si tu, hali zinazohusiana na asili, uwezo, jinsia, mwelekeo wa kijinsia, dini, kabila na/au utaifa/taifa la asili.

Lazima washiriki wawe na uwezo wa kuzungumza na kusoma mojawapo ya lugha zifuatazo: Kiarabu, Kiburma, Kidari, Kiingereza, Kinyarwanda, Kirusi, Kihispania, na/au Kiswahili.

Kiwango cha msingi cha kuelewa lugha ya Kiingereza kinapendekezwa, lakini si lazima. Huduma za ukalimani zitatolewa kama itakavyohitajika. Washiriki watarajiwa wanapaswa kutaja mapema ikiwa wanahitaji huduma za ukalimani. Pia, shirika la CORE litatoa tafsiri ya nyenzo za mafunzo kwa washiriki wapya, karatasi za kazi au hati kama itakavyohitajika.

Ili kufikia kila pembe ya Marekani, washiriki wanapaswa kuwa na uwezo wa kufanyia kazi ya RAC mtandaoni. Ingawa shirika la CORE litajitahidi kadri liwezavyo ili kushirikisha watu wenye uwezo tofauti wa masuala ya teknolojia, washiriki wanapaswa kuwa kiwango cha msingi cha ufahamu wa masuala ya teknolojia na utumiaji. Hii inajumuisha uwezo wa kujiunga katika mkutano kupitia simu au Zoom kwa kutumia simu, kompyuta kibao au kompyuta ya kawaida yenye muunganisho thabiti wa intaneti.

Washiriki watajitolea kutoa huduma kwa kipindi cha miezi 12, ambayo inajumuisha kufanya mikutano mifupi ya kila mwezi kupitia Zoom na mradi mmoja hadi miwili mikubwa kama vile kufanya mazungumzo na kikundi lengwa, mahojiano na/au kufanya majaribio ya mtumiaji.  Ili upate maelezo zaidi kuhusu miradi ambayo washiriki watafanya mwaka huu, tafadhali angalia maelezo ya kazi.

Mikutano ya kila mwezi huchukua kati ya dakika 60 hadi 90 na hufanywa mtandaoni. Tarehe na saa za mikutano ya kila mwezi zitabainishwa baada ya kufanywa kwa mashauriano kati ya washiriki na wafanyakazi wa shirika la CORE. Washiriki watapaswa kuwa na muunganisho thabiti wa intaneti na uwezo wa kutumia kompyuta au kompyuta kibao ili kuhudhuria mkutano wa mtandaoni wa Zoom, au uwezo wa kujiunga kupitia simu ya mkononi. Wakati mwingine, huenda shughuli za matayarisho zikahitajika, lakini shirika la CORE itatoa mawasiliano kuhusu shughuli zote za matayarisho kabla ya kufanywa kwa mkutano wa kila mwezi.

Ili utume maombi, fuata hatua zilizobainishwa hapa. Baada ya kupokea maombi yako, tutawasiliana nawe baadaye kwa ajili ya kufanya mahojiano ikiwa utachaguliwa kushiriki.